Naibu Rais Rigathi Gachagua amempongeza Rais William Ruto kwa kuongoza viongozi wengine wa bara la Afrika kuelezea msimamo thabiti wa bara hilo kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema Rais Ruto ameonyesha uongozi wa kuigwa kwa kuwaleta pamoja viongozi hao kuchukua msimamo wa pamoja kuhusiana na suala hilo.
Gachagua aliyasema hayo hii leo Alhamisi alipofungua maonyesho ya kilimo ya kitaifa ya mwaka huu ya Mombasa.
“Kenya sasa inaheshimika barani Afrika na duniani kwa sababu ya uongozi wa Rais wakati wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi. Tunafurahi kwamba viongozi wa afrika wametambua uongozi wa Rais wetu,” alisema Naibu Rais katika uwanja wa maonyesho ya ASK wa Mombasa mjini Nyali.
Alisema kuanzia sasa, Afrika itazungumza kwa sauti moja kuhusiana na masuala ya tabia nchi na ufadhili wa tabia nchhi.
“Rais amefanikiwa kuiunganisha Afrika kuzungumza kwa sauti moja. Wakati wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mkutano wa COP-28, Afrika itazungumza kwa sauti moja na kuwa na msimamo mmoja,” aliongeza Gachagua.
Kauli zake zikiwadia siku moja baada ya kukamilika kwa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi jijini Nairobi.
Kongamano hilo la siku tatu lililofanyika katika jumba la KICC liliwaleta pamoja Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 20 kutoka barani Afrika na maelfu ya wajumbe kutoka kote duniani.
Viongozi hao wa Afrika wameahidi kushirikiana na kuchukua msimamo wa pamoja katika masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi na ukabilianaji wa athari zake.