Afrika Mashariki Fest wapiga hatua baada ya kuwasilisha Azimio la Butiama kwa kongamano la EAC

Dismas Otuke
3 Min Read

Shirika la Afrika Mashariki Fest lenye makao yake nchini Uganda linajivunia kupiga hatua kubwa katika ajenda yake ya kuhimiza utangamano wa raia wa mataifa ya Afrika Mashariki.

Hii ni baada ya shirika hilo la vijana kupata fursa ya kuwasilisha mwafaka wa Butiama maarufu kama Azimio la Butiama, kwa Kongamano la 24 la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumamosi iliyopita mjini Arusha nchini Tanzania.

Afisa Mkuu mtendaji wa Afrika Mashariki FEST  Dkt.Ronex Kisembo Tendo, aliwasilisha mwafaka huo wa Butiama kwa viongozi kutoka mataifa  manane waliohudhuria kongamano hilo.

Kongamano la mwaka huu liliambatana na sherehe za miaka 25  tangu kubuniwa kwa EAC mwaka 1999.

Mashariki FEST iliwasilisha mwafaka huo kwa viongozi wa mataifa manane wanachama wa EAC waliohudhuria kongamano hilo la siku mbili.

Mapendekezo yaliyomo kwenye mwafaka huo ni pamoja na :-

  1. Utekelezaji wa kuwa na  itifaki ya soko moja kuimarisha biashara, usafirishaji mizigo na nafasi  za ajira
  2. Kuongeza uwekezaji utakaowezesha vijana kupitia kwa elimu, ujasiriamali, uvumbuzi, kupunguza changamoto ya kukosa ajira na kuinua uwezo wa kanda ya Afrika Mashariki.
  3. Kubaini changamoto zilizopo kama  vile mizozo, ugaidi, misukosuko ya kisiasa na kutoa mwelekeo wa kulinda na kudumisha amani na usalama wa kikanda.
  4. Kuhimiza maendeleo endelevu kupitia kwa shughuli zisizochafua mazingira, kuwa na chakula toshelezi, kupambana na mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya sarafu moja ya Jumuia ya Afrika Mashariki, usafiri mmoja wa angani na huduma moja ya mawasiliano.
  5. Kuhimiza kufurahia na kusherehekea tamaduni na turathi,  kuhumiza umoja wa lugha na kukumbatia umoja wa Kiafrika.
  6. Kutaka mataifa ya EAC kuwa na timu moja katika michezo ya kimataifa kama vile michezo ya Afrika, Olimpiki, mashindano ya Dunia na Kombe la Dunia na kutumia bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwafaka huo ulisainiwa na vijana wa kanda ya Afrika Mashariki  Oktoba 14 mwaka huu,  nyumbani kwa Rais mwanzilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Endapo mwafaka huo utazingatiwa na kutekelezwa na viongozi wanane wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huenda  raia wa mataifa hayo wakanufaika pakubwa kutokana na kutanuliwa kwa fursa za kibiashara, utangamano na ajira.

Nguzo kuu pia ya jumuiya hiyo ni matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa mataifa yote kama lugha rasmi ya mawasiliono.

Haya yanajiri wakati ambapo Uganda imetwikwa  jukumu la kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili  mwezi Aprili mwaka ujao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *