Taifa la Afrika Kusini limewasilisha rufaa dhidi ya Israel katika mahakama ya makosa ya jinai ICC ikitaka ichunguzwe kwa makosa ya kivita.
Rais Cyril Ramaphosa alisema kwamba Afrika Kusini inaamini kwamba Israel inatekeleza makosa ya kivita na mauaji ya halaiki katika ukanda wa Gaza.
Wabunge wa Afrika Kusini walifaa kujadili mjadala wa kutafuta kufungwa kwa ubalozi wa Israel nchini humo na kukatizwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo leo Alhamisi, Novemba 16, 2023.
Ramaphosa ameelezea kwamba hatua yao imechochewa na idadi kubwa ya Wapalestina ambao wameuawa huko Gaza pamoja na miundomsingi iliyoharibiwa zikiwemo hospitali.
Alikuwa akizungumza huko Qatar ambapo anaendeleza ziara ya kikazi ambapo alifafanua kwamba hawaungi mkono kamwe mashambulizi yaliyotekelezwa na Hamas awali na kusababisha Israel kushambulia Gaza.
Chama cha Rais Ramaphosa cha African National Congress ANC kilitangaza kwamba kitaunga mkono mjadala huo uliowekwa bungeni na chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters EFF kuhusu kufungwa kwa ubalozi wa Israel nchini Afrika Kusini.