Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma imepinga kuachiliwa kwa Ian Njoroge kwa dhamana ikisema kwamba hatua ya kunyimwa dhamana itakuwa funzo kwa watu kuhusu matokeo ya kushambulia maafisa wa polisi na maafisa wengine wa umma.
DPP kupitia taarifa leo, ilielezea kwamba ili haki ipatikane, ni vizuri mtu asipatiwe dhamana iwapo kosa lake ni kubwa.
Njoroge ameshtakiwa kwa wizi wa kimabavu, ambapo Victor Owiti, James Gachoka na Virginia Kariuki wa upande wa masktaka waliambia hakimu Ben Mark Ekhubi jana kwamba kuna sababu za kutosha za kumnyima mshukiwa dhamana.
Walisisitiza kwamba makosa yake ni makubwa na kuelezea kwamba alishambulia afisa wa polisi wa umri wa miaka 57 kando na ukweli kwamba amewahi kushtakiwa na kufikishwa mahakamani mara mbili kwa makosa ya trafiki na ya uhalifu.
Sababu nyingine iliyotajwa na upande wa mashtaka ya kumnyima Ian dhamana ni uwezekano wa kujificha alivyofanya baada ya kushambulia afisa huyo na video ikasambazwa mitandaoni.
Wanahisi pia kwamba huenda akavuruga ushahidi ikitizamiwa kwamba kuna ripoti mitandaoni kwamba afisa wa polisi aliyeshambuliwa amekubali kumsamehe.
Mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi la Ian la kuachiliwa kwa dhamana kesho Juni 7, 2024.