Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imemkamata afisa wa polisi kwa madai ya kushiriki ufisadi.
Koplo Kennedy Monyo Wawere ambaye anafanya kazi katika Halmashauri ya Barabara Kuu (KeNHA) kwenye kituo cha kupima uzani wa magari cha Isinya, alikamatwa baada ya EACC kupokea malalamishi Oktoba 2, 2026, kwamba afisa huyo aliitisha hongo ya shilingi 60,000 ili abadilishe mashtaka ya mlalamishi.
EACC ilisema kuwa afisa huyo alikusudia kubadilisha kesi ya mlalamshi kutoka ile ya kuepuka kituo cha kupima uzani wa magari, hadi kosa la kukataa kusimama.
“Kufuatia uchunguzi wa malalamishi dhidi ya afisa huyo, EACC ilimkamata Cpl. Kennedy Waweru mnamo Oktoba 5, 2026 baada ya kudaiwa kupokea hongo ya shilingi 60,000,” ilisema EACC kwenye ukurasa wa X.
Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, akisubiri kukamilika kwa uchuguzi.