Tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi EACC, imemkamata afisa wa polisi wa trafiki Dobin Peter Naibei wa kituo cha polisi cha Shauri Moyo, baada ya kufumaniwa akipokea hongo.
kulingana na taarifa ya tume hiyo, Naibei alikuwa amemtia nguvuni dereva na gari lake kwa madai kwamba gari lake halikuwa na bima na alitaka hongo ili amuachilie huru.
Mlalamishi huyo alikataa kumpa hongo na badala yake alipiga ripoti kwa tume ya EACC, ambayo ilifanya operesheni na kumtia nguvuni afisa huyo.
Alikamatwa Alhamisi usiku na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, huku akisubiri hatua zaidi kuchukuliwa na tume hiyo.
Kulingana na tume hiyo, afisa huyo anakabiliwa na kosa la kupokea hongo kinyume na sehemu ya 6(1) (a) kulingana na sehemu ya18 ya sheria kuhusu hongo ya mwaka 2016.
Akithibitisha kisa hicho, msemaji wa tume ya EACC Eric Ngumbi, alisema tume hiyo imeimarisha msako katika barabara kuu kote nchini hasaa wakati huu wa msimu wa krisimasi, ili kukabiliana na visa vya ufisadi.