Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wamemkamata afisa wa kampuni ya maji na majitaka ya Nakuru (NAWASCO) kwa madai ya ufisadi.
Leonard Cheruiyot Mutai alikamatwa Machi 23, 2026 baada ya malalamishi kutoka kwa mteja aliyedai kuwa afisa huyo aliitisha hongo ya shilingi 15,000 katika mtaa wa Langa Langa.
Kupitia ukurasa wake wa X, EACC imesema maafisa wake walitekeleza operesheni iliyofanikisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo akipokea hongo.
Alipokamatwa, mshukiwa alipatikana na shilingi 15,000 pesa taslimu, shilingi 100,000 kwenye soksi na shilingi 18,000 ndani ya koti lake.
Mshukiwa alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Central Nakuru na kisha kuachiliwa kwa dhamana ya polisi ya shilingi 20,000 akisubiri kukamilika kwa uchunguzi.