Afisa wa IEBC akamatwa kwa kughushi vyeti vya masomo

Tom Mathinji
2 Min Read
Caroline Sabiri Manyange.

Tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi EACC, leo Jumatatu imemkamata afisa mmoja mkuu wa tume ya uchaguzi nchini IEBC, ambaye anadaiwa alighushi vyeti vyake vya masomo, na kuvitumia kutafuta ajira katika tume hiyo Aprili 4, 2012.

Msemaji wa EACC Eric Ngumbi, alithibitisha kuwa Caroline Sabiri Manyange,alikamatwa akiwa nyumbani kwake katika mtaa wa  Nairobi West, na kupelekwa katika kituo cha polisi kilichoko katika makao makuu ya EACC kuhojiwa zaidi.

Kulingana na EACC, Manyange atafikishwa katika mahakama za kukabiliana na ufisadi za Milimani Jijini Nairobi.

EACC ilisema kuwa mshukiwa huyo alighushi cheti za shahada ya uzamili ya somo kuhusu idadi ya watu, akidai kuwa alihitimu katika chuo kikuu cha Nairobi Mei 9, 2004 na kuitumia kupandishwa cheo katika tume ya IEBC.

Manyange anadaiwa kupokea mshahara na marupurupu kutumia cheti hicho ya zaidi ya shilingi milioni 37, na hivyo kushtakiwa na kosa la kujipatia mali ya umma kinyume na sheria.

Mshukiwa huyo alikamatwa baada ya kiongozi wa mashtaka ya umma kukubaliana na mapendekezo ya EACC, kwamba afunguliwe mashtaka ya kughushi kinyume na sehemu ya 345 pamoja na ile ya 349 ya katiba, na pia shtaka la kutumia vyeti bandia kinyume na sehemu ya 353 ya katiba.

EACC pia itawasilisha kesi mahakamani ili kutwaa mishahara na marupurupu ya shilingi milioni 37, alizopokea mshukiwa huyo kutumia vyeti bandia.

TAGGED:
Share This Article