Afisa wa chuo kikuu akamatwa kwa kuitisha hongo

Tom Mathinji
1 Min Read
Afisa wa ICT akamatwa kwa kuitisha hongo.

Maafisa wa tume ya Maadili na kukabiliana na ufisadi hapa nchini EACC, wamemkamata afisa wa chuo kikuu cha Cooperative, kwa kuitisha hongo ya shilingi 50,000, ili arekebishe kasoro za matokeo ya mtihani ya mwanafunzi, kabla ya sherehe za mahafali mwezi Disemba mwaka huu.

Mshukiwa huyo Evans Matiro Watenya, alidaiwa kuitisha hongo hiyo, ili arekebishe kasoro ya matokeo ya mtihani ya mwanafunzi, iliyonakiliwa katika tovuti ya chuo hicho.

Kulingana na  EACC, mwanafunzi huyo ambaye awali alipata alama za Second Class Honours Upper Division, aligundua kuwa amepewa alama za Second Class Honours Lower Division.

Mwanafunzi huyo alipofika katika afisi za idara ya teknolojia ya habari na mawasiliano ICT ya chuo hicho, Watenya alimfahamisha kuwa kasoro hiyo inaweza rekebishwa iwapo atatoa hongo ya shilingi 50,000.

Aliposhindwa kupata fedha hizo, mwanafunzi huyo alipiga ripoti katika afisi za EACC.

Tume hiyo ilithibitisha madai hayo na kuanzisha operesheni mara moja, na kumkamata mshukiwa huyo Ijumaa jioni katika chuo hicho kikuu, alipokubali malipo ya awali ya shilingi 30,000.

Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, akisubiri kufikishwa mahakamai.

TAGGED:
Share This Article