Senegal imewaita wachezaji sita wa Ligi Kuu pamoja na Sadio Mane kwa ajili ya kutetea ubingwa wao wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast mwezi ujao.
Wachezaji wawili wa Nottingham Forest Moussa Niakhate na Cheikhou Kouyate, beki wa Fulham Fode Ballo-Toure, kiungo wa Tottenham Pape Matar Sarr, Idrissa Gueye wa Everton na mshambuliaji wa Chelsea Nicolas Jackson wote wamejumuishwa katika timu ya taifa ya Teranga Lions na kocha Aliou Cisse.
Kipa wa Middlesbrough Seny Dieng na mshambuliaji wa Rangers Abdallah Sima pia wako kwenye kikosi cha wachezaji 27.
Fainali za Afcon 2023 – zimetangazwa rasmi kuwa hivyo ingawa zinachezwa 2024 – zitaanza Januari 13, na fainali mnamo 11 Februari.
Mshambulizi wa zamani wa Liverpool, Mane, ambaye sasa anachezea klabu ya Saudi Arabia ya Al Nassr, alifunga penalti ya ushindi katika mikwaju ya penalti dhidi ya Misri katika fainali ya Kombe la Mataifa ya 2021 na kutwaa taji la kwanza la wakubwa la Senegal.
Nchi 24 zinazoshindana zina hadi Januari 3 kutaja vikosi vyao vya mwisho.