Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani ametoa wito wa kuongezwa kwa utambuzi na msaada kwa wanawake kama nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Gavana huyo alikuwa akizungumza katika hafla ya kufunga awamu ya nne ya kongamano la “What Women Want 2026” iliyofanyika kwenye mkahawa wa Trademark jijini Nairobi.
Alisema ni wakati wa washikadau kuwekeza zaidi katika kuwawezesha wanawake hasa katika ngazi za mashinani akisisitiza mchango mkubwa wa wanawake katika uongozi, ujasiriamali na maendeleo ya jamii.
Achani ameeleza kuwa kaunti ya Kwale imepiga hatua katika kuwawezesha wanawake na vijana kwa kusajili zaidi ya kampuni 400 zinazomilikiwa na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, huku zaidi ya kampuni 200 tayari zikinufaika na zabuni za kaunti.
Gavana Achani aidha ameongeza kuwa kupitia mfuko wa Revolving Fund, serikali ya kaunti ya Kwale inaendelea kutoa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ili kuimarisha uchumi wa kaunti hiyo.