Halmashauri ya Kupambana na Bidhaa Ghushi (ACA), imegundua sakata ya upakiaji wa mbolea bandia inayojumuisha ile ya gharama nafuu inayotolewa na serikali katika eneo la Matungu, kaunti ya Kakamega.
Operesheni hiyo ilisababisha kupatikana kwa magunia 323 ya mbolea bandia iliyopakiwa kwa njia haramu yenye thamani ya shilingi milioni 1.6, malori mawili na vifaa vya viwanda vya upakiaji vinavyoshukiwa kutumika kwenye sakata hiyo.
Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa mbolea hiyo iliporwa kutoka kwa ule mpango wa serikali wa mbolea ya gharama nafuu na ukapakiwa upya kwa kutumia nembo ya kampuni ya Falcon, kwa lengo la kuwauzia wakulima kwa bei ya kawaida sokoni.
Madereva wawili wa malori hayo walikamatwa kwenye operesheni hiyo, na wanawasaidia polisi kwa uchunguzi, huku polisi wakiwasaka watu wengine wanaoshukiwa kuhusika katika sakata hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa ACA, Robi King’a alisisitiza haja ya kudumisha maadili ya usambazaji wa bidhaa za kilimo na kuwalinda wakulima dhidi ya wafanyabiashara walaghai.