Abitex ahisi kwamba King Saha alipendelewa na UPDF

Anashangaa jinsi Saha ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali, alikubaliwa na jeshi linalosimamia uwanja wa Kololo kufanya maandalizi ya mapema huko.

Marion Bosire
2 Min Read
King Saha

Mwandaaji wa tamasha nchini Uganda Abbey Musinguzi maarufu kama Abitex anahisi kwamba mwanamuziki King Saha, alipendelewa na jeshi la nchi hiyo UPDF kuhusu matumizi ya uwanja wa Kololo.

Akizungumza kwenye mahojiano, Abitex alishangaa jinsi Saha ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali, alikubaliwa na jeshi ambalo linasimamia uwanja wa Kololo kufanya maandalizi ya mapema huko.

Abitex alielezea kwamba King Saha alipatiwa muda wa siku tatu kufanya maandalizi uwanjani Kololo kwa ajili ya tamasha yake ya ‘Tondeka Ekololo’ iliyofanyika Agosti 14, 2026.

Msimamizi huyo wa maonyesho, aliongeza kwamba anatilia shaka suala hilo ikikumbukwa kwamba King Saha ni msaidizi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform, NUP.

Saha alijaza Kololo Ijumaa, siku chache baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama wenye silaha wakati wa shughuli za kutangaza tamasha hiyo.

Abitex, ambaye aliandaa tamasha ya Ray G katika uwanja huo wa Kololo wiki moja kabla ya tamasha ya Saha, alidai kuwa walipatiwa siku moja tu kufanya maandalizi tena usiku.

Alikiri kwamba Saha amewazidi waandaaji wengine katika kupata ruhusa ya kutumia uwanja huo na akaahidi kutafuta maelezo kutoka Wizara ya Ulinzi.

Aliongeza kuwa King Saha ndiye aliyeomba ukumbi huo, bila hata kuwa na uhakika kama angepewa, lakini jeshi la taifa la Uganda lilichukua udhibiti kamili wa tamasha hiyo nzima.

Share This Article