Abel Mutua aahidi kusimulia kuhusu kifo cha kakake

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji Abel Mutua ameahidi kusimulia kuhusu kifo cha kakake mdogo kwa jina Raphael Mbuvi Musyoka ambaye alifariki Disemba 28, 2023.

Alichapisha picha ya gari la polisi kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii akisema, ” Ndani ya hili gari umelazwa mwili wa jamaa ambaye wakati mmoja alikuwa mahiri na ambaye maisha yake yamekatizwa kwa njia ya kusikitisha akiwa na umri wa miaka 23.”

Aliendelea kusema kwamba walijaribu kadri ya uwezo wao kumsaidia lakini labda juhudi zao hazikutosha.

Abel anasema anaamini historia ya Raphael ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 23 itaokoa watu fulani ndiposa anapanga kuitoa.

Mutua ambaye pia ni mwandishi stadi wa miswada ya maigizo ameomba usaidizi wa kifedha mitandaoni ili kumwandalia kakake mazishi faafu.

Ombi la Mutua lilizua hisia mseto kati ya wafuasi wake mitandaoni wengine wakihisi kwamba ana uwezo wa kifedha wa kuandalia kakake mazishi na wengine wakimuunga mkono.

Kupitia mtandao wa X, Abel ameshukuru wanaomwonyesha upendo wakati huu wa majonzi akisema wengine wanafahamu kilichotokea tangu kakake alipogonjeka na atahadithia.

Abel analia akisema haamini talanta ya Raphael katika soka imeangamia bila kutumika ipasavyo.

Share This Article