Serikali yaongeza muda wa agizo la kusimamisha kusailiwa upya kwa madereva

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali kupitia kwa wizara ya uchukuzi imeongeza muda wa agizo lililosimamisha mpango wa kuwasaili upya waendeshaji magari ya uchukuzi wa umma na mengine ya biashara.

Kupitia taarifa iliyotiwa saini na waziri wa uchukuzi na barabara Kipchumba Murkomen, serikali imeongeza muda wa agizo hilo kwa miezi mitatu kutoka tarehe ya taarifa ya waziri ambayo ni Oktoba 6, 2023.

Mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarani ilikuwa imetangaza sharti jipya mwezi Julai kwamba kila dereva asailiwe upya kabla ya kuongezewa muda wa matumizi ya leseni ya uendeshaji gari.

Madereva wa magari ya uchukuzi wa abiria na mengine ya kibiashara walitoa ilani ya mgomo Julai 12, 2023 kama hatua ya kupinga sharti hilo jipya la NTSA. Walilitaja kuwa la kibaguzi.

Baadaye waziri Murkomen alitangaza kusimamishwa kwa utekelezaji wa sharti hilo hadi Septemba Mosi 2023 ili kutoa nafasi kwa kubuniwa kwa kamati ya wadau wote husika kutafuta namna ya kushughulikia suala hilo.

Takwimu za NTSA za usaili wa madereva wazoefu 1847 uliofanyika mwezi Juni zinaonyesha kwamba ni madereva 576 pekee waliopita majaribio ya ufaafu wao kama madereva.

Ugunduzi huo ulisababisha NTSA kufanya iwe lazima kwa madereva hao kusailiwa kila baada ya miaka mitatu kabla ya kuongezewa muda wa leseni zao.

Waziri Murkomen kwenye taarifa yake alielezea kwamba hatua ya kuongeza muda wa kusimamisha utekelezaji wa sharti jipya la NTSA inadhamiriwa kutoa muda zaidi kwa kamati iliyobuniwa kushughulikia malalamishi ya madereva na kubuni njia mwafaka ya kuhakikisha madereva wanahitimu kuwa barabarani.

Website |  + posts
Share This Article