Mashindano ya riadha ya wakongwe yaandaliwa Nandi

2 Min Read

Shirika moja lisilokuwa la serikali la Agui Kogo linalotoa huduma kwa wakongwe katika kaunti ya Nandi.

Liliandaa mashindano ya riadha katika eneo la Tindiret kama njia ya kuhamasisha umma kusaidia wazee kwani wengi wao wanaishi kwa upweke baada ya familia zao kuwaacha na kwenda kujitafutia riziki.

Walioshiriki mashindano hayo ni wazee wa umri wa miaka 70 hadi 100 na washindi walizawadiwa pesa na blanketi. Walipokea pia matibabu ya bure na chakula cha mchana.

Kasisi Augustine Baren ambaye ni mwazilishi wa shirika hilo alisema wamejaribu kufikia serikali ya Nandi ili kupata msaada bila mafanikio. Sasa wanataka serikali kuu iingilie kati ili wazee wengi wanufaike na mpango huo.

Truphena Korir, mmoja wa madaktari wa kujitolea katika shirika hilo, anasema kufikia sasa, wamesaidia wazee zaidi ya 1,000 katika kaunti hiyo.

Misaada wanayotoa kwa wakongwe ni kama chakula, mavazi na huwa wanajengea wengine nyumba. Wanaitaka serikali isajili wakongwe hao kwenye bima ya kitaifa ya matibabu ya NHIF.

Erick Barangetuny naye anaitaka serikali iongeze pesa ambazo wazee wa eneo hilo hupokea kutoka kwa serikali hasa wanaoishi katika maeneo tengwa na yaliyosalia nyuma kimaendeleo.

Washiriki wa mbio hizo nao walipendekeza kwamba pesa hizo ziongezwe kutoka elfu mbili kila mwezi hadi elfu 10 kwa mwezi ili waweze kujikimu kimaisha.

Website |  + posts
Kimutai Murisha
Share This Article