Kampuni ya Kenya Pipeline imemthibitisha Pius Mwendwa kuwa Mkurugenzi Mkuu na Afisa Mkuu Mtendaji, ikisema anaanza kutekeleza majukumu yake mara moja.
Uteuzi wa Mwendwa unajiri baada ya mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo, iliyoandaliwa siku ya Alhamisi.
Mwendwa amekuwa akikaimu wadhifa huo tangu tarehe 8 mwezi Aprili mwaka 2026, baada ya kuondoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Joe Sang aliyekuwa akichunguzwa kwa madai ya usambazaji na uagizaji wa mafuta.
Kwenye tangazo kwa umma, kampuni hiyo ilisema Mwendwa alijiunga na KPC mwezi Agosti 2010 na kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika masuala ya fedha, zikiwemo Mhasibu Mkuu, Meneja wa Fedha, na Meneja Mkuu wa Fedha.
Mwendwa Ana shahada ya uzamili ya Biashara na shahada ya kwanza ya Biashara kuhusu Fedha.
Kabla ya kujiunga na KPC, Mwendwa alifanya kazi katika Shirika la Habari la Nation Media Group kwa zaidi ya miaka 10.