Takriban watu 31 wamefariki na wengine 21 kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa limebeba bidhaa za mafuta kupinduka na kushika moto jijini Cairo, nchini Misri Jumatano.
Moto huo ulizuka juu ya handaki katika eneo la al-Warak, wilaya ya Imbabah, Giza. Barabara husika inaunganisha barabara kuu muhimu katika eneo la Greater Cairo, ikihudumia magavana wa Cairo, Giza na Qalyubia.
Vyombo vya habari vya nchini humo viliripoti kuwa lori hilo lilipoteza mwelekeo, kugonga kizuizi cha katikati ya barabara na kupinduka, hali iliyosababisha mlipuko. Moto huo ulizimwa baadaye.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Misri ametangaza uchunguzi kuhusu ajali hiyo na kuagiza sampuli za vinasaba kuchukuliwa kutoka kwa miili ya waathiriwa. Ofisi hiyo pia ilisema magari 27 yaliteketea kwa moto.
Wizara ya Afya ilisema ambulansi 39 zilitumwa eneo la tukio, huku waliojeruhiwa wakipelekwa kwenye hospitali za karibu kwa matibabu.
Waziri wa Afya Khaled Abdel Ghaffar alisema atazuru eneo la ajali binafsi.
Msemaji rasmi wa Ikulu ya Misri alisema Rais Abdel Fattah el-Sisi ametoa rambirambi zake kwa familia za waliofariki na kuwatakia majeruhi nafuu ya haraka.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mawaziri, Waziri Mkuu Mostafa Madbouly pia alitoa pole kwa familia zilizoathirika na kuagiza serikali kugharamia matibabu ya majeruhi.
“Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo na kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha waliojeruhiwa wanapata huduma muhimu za matibabu,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.