Rais Ruto azindua ujenzi wa kiwanda cha mkaa cha Bamburi

Mradi huo utaongeza uwezo wa kampuni kuzalisha mkaa au clinker kutoka tani milioni moja hadi milioni 2.6 kwa mwaka.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumanne, Novemba 24, 2026, aliweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mkaa unaotumika kutengeneza simiti almaarufu Clinker.

Kiongozi wa nchi alisema uwekezaji huo utaimarisha uzalishaji wa saruji nchini na kutengeneza nafasi za ajira kwa wakazi wa eneo hilo.

Kiwanda hicho kipya cha kampuni ya Bamburi Cement mjini Matuga, Kaunti ya Kwale, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 5,000 za clinker kwa siku, sawa na takribani tani milioni 1.6 kwa mwaka.

Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Bamburi Cement inayomilikiwa na Amsons Group utaongeza uwezo wa kampuni kuzalisha clinker kutoka tani milioni moja hadi milioni 2.6 kwa mwaka.

Uzalishaji wa saruji pia utaongezeka kutoka tani milioni 1.8 hadi milioni nne kwa mwaka.

Ruto alisema uzalishaji wa clinker nchini utapunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni na kuimarisha sekta ya viwanda.

Alitoa wito kwa kampuni hiyo kuwapa kipaumbele vijana wa eneo hilo katika ajira na mafunzo ya ujuzi, pamoja na kuwapa wafanyabiashara nafasi za kusambaza bidhaa na huduma.

Alitaja maeneo ya Matuga, Kinango, Msambweni na Lunga Lunga kuwa miongoni mwa maeneo yatakayofaidika kupitia ajira, kandarasi na fursa za kibiashara.

Uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za serikali kupanua uzalishaji wa ndani, sambamba na miradi mingine ya clinker katika kaunti za West Pokot na Kitui.

Share This Article