Koffi Olomide kusherehekea miaka 40 ya bendi yake

Atazindua albamu mpya iitwayo La Vie en Rose, ambayo ina jumla ya nyimbo 33, Alhamisi, Novemba 26, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki nguli wa Congo Koffi Olomidé anapanga kusherehekea miongo minne ya safari yake ya muziki na uwepo wa bendi yake iitwayo Quartier Latin.

Atafanya hivyo kwa kuzindua albamu mpya iitwayo La Vie en Rose, ambayo ina jumla ya nyimbo 33, Alhamisi, Novemba 26, 2026.

Tarehe ya uzinduzi huo ina maana kubwa kihistoria kwani inasadifiana na tarehe ya kuanzishwa kwa bendi ya Quartier Latin International, Novemba 26, 1986.

Kwa miaka 40 iliyopita, bendi ya Quartier Latin imekuwa nguzo muhimu katika muziki wa Afrika, ikichangia pakubwa kuutangaza muziki wa rumba wa asili ya Kongo na ndombolo duniani.

Bendi hiyo pia ilikuwa chachu ya ujio wa nyota wakubwa wa muziki Fally Ipupa na Ferré Gola.

Albamu mpya ya “La Vie en Rose” ni ya kwanza kurekodiwa kwa pamoja na wanachama wote wa bendi hiyo na kutolewa rasmi chini ya jina lake katika kipindi cha miaka 20.

Albamu yao ya mwisho ya aina hiyo ilikuwa “Danger de Mort”, iliyotolewa mwaka 2006.

Kuadhimisha hatua hiyo muhimu, Koffi Olomidé, maarufu kama Le Grand Mopao, amewaunganisha wanamuziki wa sasa wa bendi hiyo na wa awali.

Kabla ya albamu hiyo kutoka, Koffi alidokeza orodha ya nyimbo zitakazowashirikisha wasanii mbalimbali, akiwemo mshirika wake wa muda mrefu Cindy Le Cœur, ambaye ametengewa wimbo maalumu wa heshima unaoitwa “Cindy d’Or”.

Albamu hiyo pia inatarajiwa kuwa mwanzo rasmi wa maandalizi ya ziara yake ya kimataifa ya kuaga mashabiki inayotarajiwa kufanyika mwaka 2027.

Share This Article