Uingereza imetangazwa kuwa mwenyeji wa michuano kuwania Kombe la Dunia la Soka la Wanawake mwaka 2035, kwenye uamuzi uliotangazwa matika mkutano wa FIFA ulioandaliwa Zurich, Uswizi siku ya Jumatatu.
Mashindano hayo ni ya kwanza ya kombe la dunia la FIFA kuandaliwa nchini Uingereza, tangu mwaka 1966.
Uingereza inalenga kutumia viwanja 22 katika miji 16, vikiwemo viwanja 16 nchini England, vitatu Wales, viwili Scotland na kimoja Ireland Kaskazini.
Mashirikisho manne yatashirikiana kuandaa michuano hiyo ambayo ni Chama cha Soka cha England (FA), Chama cha Soka cha Ireland (Irish FA), Chama cha Soka cha Scotland (Scottish FA) na Chama cha Soka cha Wales (FA of Wales).
Aidha, mashindano hayo yanalenga kutoa jukwaa kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa michezo ya wanawake nchini Uingereza, kuendeleza usawa wa kijinsia katika michezo na jamii, pamoja na kuchochea ukuaji wa michezo ya wanawake kwa kizazi kijacho.
FIFA inatarajiwa kuthibitisha baadaye miji itakayokuwa mwenyeji, viwanja vitakavyotumika pamoja na vituo vya mazoezi ya timu zitakazoshiriki.
Wakati huo huo, FIFA imetanagaza kuwa mashindano ya kuwania Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2031, yataandaliwa kwa pamoja na Marekani, Mexico, Costa Rica na Jamaica.