KRA yafutilia mbali shilingi bilioni 64, walipa ushuru 900,000 wanufaika

Mpango huo ambao unalenga walipaji ushuru walio na malimbikizi ya kodi, pia umewezesha serikali kukusanya shillingi Bilioni 29.1 zilizokuwa zikidaiwa walipaushuru.

Tom Mathinji
1 Min Read
Makao Maku ya KRA Jijini Nairobi.

Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini Kenya, imesema Wakenya  984,489 wamenufaika na mpango wa sasa wa msamaha ambapo adhabu, faini na riba za kitita cha shilingi bilioni 64.39 zimefutiliwa mbali.

Mpango huo ambao unalenga walipaji ushuru walio na malimbikizi ya kodi, pia umewezesha serikali kukusanya shillingi Bilioni 29.1 zilizokuwa zikidaiwa walipaushuru, ikitoa msamaha kwa watu na biashara katika juhudi za kuwaondolea madeni ya ushuru.

Kwenye taarifa, kamishna wa KRA anayehusika na walipaji ushuru wa kiwango kikubwa na cha kadri, Weldon Ng’eno, alisema halmashauri hiyo imeondoa riba za shilingi bilioni 31.9, adhabu za jumla ya shilingi bilioni 32.5 pamoja na faini za shilingi Milioni 11.5 kufikia Novemba 16 mwaka huu.

Ng’eno alisema hatua hiyo iliashiria wajibu wa mpango huo wa kuwasaidia walipaji ushuru kulipa madeni yao huku pia ukiwahimiza wakenya kujinufaisha na kipindi hicho cha msamaha ambacho kitakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Hatua hii inaashiria jukumu la halmashauri hii kuwasaidia walipa ushuru kushughulikia malimbikizi yao ya ushuru na kutoa fursa kwa wengine kunufaika kabla ya makataa ya tarehe 31 Disemba 2026,” alisema Ng’eno.

Share This Article