Mwigizaji wa Tanzania Jackline Wolper amefichua kwamba tayari amemwomba mume wake Rich Mitindo talaka ila hajampa.
Akizungumza kwenye mahojiano, mrembo huyo ambaye pia ni mfanyabiashara alisema kwamba tofauti zilizopo kati yao haziwezi kusuluhishwa.
Wolper anasema kwamba Rich Mitindo ambaye kwa sasa wametengana hawezi kubadilika na tayari amefanya uamuzi wa kumuacha aendelee na watu anaowataja kuwa anaowapendelea.
Kulingana naye, wamefanya vikao vya kusuluhisha tofauti zao kanisani na hata kwa wazee lakini imeshindikana kabisa.
Alipoulizwa kuhusu tatizo la kugawana mali ambalo huenda likatokea katika mchakato wa talaka, Wolper alifafanua kwamba yeye na Rich hawajawekeza pamoja, isipokuwa kwenye biashara ya suti ambayo kulingana naye imeanguka.
Lakini tena alimtetea baba huyo wa watoto wake akisema kwamba hana uchu wa mali na kamwe hajawahi kuonyesha kwamba anatamani mali yake labda kwa sababu anafahamu ni ya wanao.
Kuhusu kuendelea na maisha yake ya mahusiano, Jackline alisema wapo watu wanaotaka kuwa naye lakini anajizuia kwa sababu ya heshima kwa Rich kwani bado hajampa talaka.
Jackline Wolper na Rich Mitindo walichumbiana Agosti 2021, wakafanya harusi Novemba 19, 2022 huku taarifa za utengano zikijiri Januari 2025.
Wana watoto wawili Pascal ambaye ni mvulana aliyezaliwa mwaka 2021 na msichana aitwaye Paris aliyezaliwa mwaka 2022.
Kabla ya kuolewa na Rich Mitindo, Wolper aliwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Harmonize mwaka 2016 kabla ya kutengana mwaka 2017 kisha akawa na Diamond Platnumz.