Rais William Ruto ameendeleza uzinduzi wa miradi ya maendeleo Magharibi mwa nchi, ambako alizindua uwekaji lami barabara ya kilomita 22 ya Khayega-Malimili-Shimanyiro, katika eneo bunge la Shinyalu.
Ujenzi wa barabara hiyo utagharimu kitita cha shilingi bilioni 1.3.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila sehemu ya nchi ya Kenya inaunganishwa kupitia miundombinu ya barabara, na hakuna eneo litaachwa nyuma. Usawa ni Sawa,” alisema Rais Ruto.
Wakati huo huo Rais Ruto aliweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika kaunti ya Kakamega, utakaogharimu shilingi bilioni 2.2.
Akiwa katika kaunti hiyo ya Kakamega, kiongozi wa taifa alizindua mradi wa uunganishaji umeme wa Last Mile, akidokeza kuwa serikali itatu,ia shilingi bilioni 2.4 kuunganisha nyumba za ziada 35,000 na umeme katika kaunti hiyo.
Katika kaunti ya Busia kiongozi wa taifa alizindua ujenzi wa madarasa na afisi za shule ya upili ya ACK Musoma Senior School, katika eneo bunge la Budalangi, kaunti ya Busia.
“Tutaongeza ufadhili wa shilingi milioni 5 ili kununua vifaa vya shule hii ili kuimarisha viwango vya masomo,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto yuko kwenye ziara ya siku nne Magharibi mwa Kenya.