Jaji Mkuu Martha Koome amehimiza kuimarishwa kwa viwango vya kitaaluma katika sekta ya usuluhishaji nchini Kenya.
Alisisitiza umuhimu wa mafunzo bora, ithibati inayozingatia uwezo, ushauri elekezi na uwajibikaji ili kuboresha utatuzi wa migogoro.
Akizungumza wakati wa kuzindua Mpango Kazi wa Usuluhishaji wa Idara ya Mahakama, Mkataba wa Huduma za Usuluhishaji na Muhtasari wa Kesi za Usuluhishaji, Koome alisema kuongezeka kwa matumizi ya usuluhishaji kunapaswa kuambatana na wataalamu wenye uwezo, ithibati inayoaminika na uzingatiaji wa maadili ya taaluma.
Alisisitiza kuwa kuimarisha taaluma ya usuluhishaji hakupaswi kuzuia wataalamu kutoka sekta nyingine kushiriki, akibainisha kuwa usuluhishaji unahitaji ujuzi kutoka nyanja mbalimbali zikiwemo saikolojia, biashara, uhandisi, benki na huduma za kijamii.
Koome pia alitoa wito wa kuanzishwa kwa mifumo endelevu ya ufadhili nje ya bajeti ya Idara ya Mahakama ili kuwasaidia wasuluhishaji na kuhakikisha makundi maskini na yaliyo katika mazingira magumu yanapata haki.
Alihimiza taasisi za serikali, sekta binafsi, mashirika ya kitaaluma na washirika wa maendeleo kuunga mkono ukuaji wa usuluhishaji.
Aidha, alisema mafanikio ya usuluhishaji hayapaswi kupimwa kwa idadi ya migogoro inayomalizika kwa makubaliano pekee, bali pia utekelezaji wa makubaliano, kuridhika kwa wahusika, gharama na haki.