Dangote afanya majadiliano ya kibiashara nchini Uganda

Ziara hiyo inafuatia ujumbe wa serikali ya Uganda kutembelea viwanda vya Dangote huko Lekki, jijini Lagos, nchini Nigeria, Novemba 14.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkwasi na mwanabiashara nguli kutoka Nigeria, Aliko Dangote, yuko nchini Uganda kwa mazungumzo ya uwekezaji na Rais Yoweri Museveni.

Serikali ya taifa hilo, inamshawishi awekeze katika miradi mikubwa ya viwanda, kama kiwanda cha kusafisha mafuta cha Hoima.

Dangote aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe jana Novemba 17, ambapo alipokelewa na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ubinafsishaji na Uwekezaji, Hajjat Aminah Mukalazi, kabla ya kukutana na Museveni katika Ikulu ya Entebbe.

Ziara hiyo inafuatia ujumbe wa serikali ya Uganda kutembelea viwanda vya Dangote vya kusafisha mafuta na kuzalisha mbolea vilivyoko eneo la Lekki, jijini Lagos, nchini Nigeria, Novemba 14.

Uganda inataka Kampuni ya Dangote ishiriki miradi kadhaa iliyopendekezwa, kama ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta huko Hoima chenye uwezo wa kuchakata mapipa 60,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

Kwa mujibu wa Dangote Group, mazungumzo hayo pia yalijikita katika upanuzi wa viwanda, uhamishaji wa teknolojia na ushirikiano wa uwekezaji.

Mukalazi alisema uzoefu wa Dangote katika kufadhili, kujenga na kuendesha viwanda vikubwa unaweza kusaidia Uganda kuongeza thamani ya rasilimali zake za asili.

Hata hivyo, mapendekezo hayo yanahitaji tathmini ya kitaalamu kutoka kwa timu ya Dangote.

Serikali inatarajia miradi hiyo itazalisha ajira, kuimarisha viwanda vya ndani na kufungua fursa za kibiashara kwa kampuni za Uganda.

Share This Article