Wasanii tisa wa muziki kutoka Afrika wameteuliwa kuwania Tuzo za 69 za Grammy, wakitambuliwa katika vipengele mbalimbali.
Tems wa Nigeria anaongoza kwa teuzi nyingi miongoni mwa wasanii wa Afrika, akiwa na jumla ya teuzi nne kufuatia kutangazwa kwa orodha hiyo Jumatatu, Novemba 16, 2026.
Wimbo wake ‘What You Need’ umeteuliwa katika vipengele vya Utendaji Bora wa R&B wa Msanii Binafsi na Wimbo Bora wa R&B, huku ‘Big Daddy’ ukiteuliwa katika kipengele cha Wimbo Bora wa Muziki wa Kiafrika. Mradi wake ‘Love Is a Kingdom’ pia umeteuliwa katika kipengele cha Albamu Bora ya Muziki wa Dunia.
Kipengele cha Albamu Bora ya Muziki wa Dunia kina wasanii wanne wa Afrika kati ya watano walioteuliwa, Ayra Starr kupitia ‘Starrgirl’, Davido na albamu yake ‘Oriadé’, na Angélique Kidjo wa Benin, kupitia ‘HOPE!’.
Ayra Starr na Kidjo pia wamepata uteuzi kupitia wimbo wao wa pamoja ‘Aye Kan’ katika kipengele cha Wimbo Bora wa Muziki wa Kiafrika. Wengine walioteuliwa ni Asake kupitia ‘Gratitude’, Tems kupitia ‘Big Daddy’ na ‘Jogodo’ wa Asake na Wizkid.
Ghana inawakilishwa na King Ayisoba na Rocky Dawuni kupitia wimbo wao wa pamoja ‘No Tradition, No Africa’.
Burna Boy ameteuliwa katika kipengele cha Utendaji Bora wa Muziki wa Dunia kupitia ‘Dai Dai’, akishirikiana na Shakira wa Columbia. Kidjo pia ametambuliwa kupitia ‘Bando (Orchestral)’, akishirikiana na Pharrell Williams na Quavo.
Sherehe za 69 za Tuzo za Grammy zinatarajiwa kufanyika Februari 7, 2027, katika ukumbi wa Crypto.com Arena jijini Los Angeles.