Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amesema Kenya inabuni fursa mpya za kibiashara, uwekezaji na ubunifu katika Asia ya kati.
Akizungumza aliposhiriki mazungumzo na balozi wa Kazakhstan nchini Kenya Barlybay Sadykov, Mudavadi aliyepia Waziri wa Mambo ya Nje, alidokeza kuwa Kenya inalenga kufungua ubalozi wa taifa hili Jijini Astana, kubuni baraza la pamoja la biashara kati ya nchi hizo mbili na kitovu cha Majani Chai na Kahawa kutoka Kenya Jijini Astana.
“Pia tuliangazia ushirikiano katika akili mnemba, uvumbuzi wa kidijitali, teknolojia ya angani, huduma za fedha, ubadilishanaji biashara na ushirikiano wa karibu wa kidiplomasia,” alisema Mudavadi.
Kulingana na Mudavadi, ushirikiano huo utafungua soko mpya kwa bidhaa za Kenya, utavutia uwekezaji na kutoa fursa mpya kwa wafanyabiashara, wanafunzi na wabunifu wachanga.
Mudavadi alisema mkutano huo uliandaliwa ili kuangazia hatua zilizopigwa baada ya ziara ya Rais William Ruto nchini Kazakhstan mwezi Mei mwaka huu.