Cheptumo Ayabei ateuliwa Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC

Evaleen Mitei amekuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC tangu mwezi Juni 2025, wakati Nancy Macharia alipostaafu baada ya kuhudumu kwa muda wa miaka 10.

Tom Mathinji
1 Min Read
Makao Makuu ya TSC.

Cheptumo Ayabei ameteuliwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC).

Akitangaza uteuzi huo Jumatatu jioni, mwenyekiti wa TSC Jamleck Muturi, alisema Cheptumo alipata wadhifa huo baada ya kukamilika kwa mchakato wenye ushindani mkali ulioandaliwa kwa kuzingatia katiba na sheria za TSC za mwaka 2012.

Ayabei, anatarajiwa kutoa mwongozo wa kimkakati, kutekeleza sera,mipango na maswala yenye umuhimu ya tume hiyo.

Aidha, anatarajiwa kushirikiana kwa karibu na wadau wengine ili kuimarisha utaalam wa walimu, uongozi wa kitaasisi na utoaji huduma, na kuchochea mageuzi katika sekta ya elimu nchini Kenya.

Tume ya TSC ilimpongeza Ayabei baada ya kuteuliwa kwake, ikidokeza kuwa inatarajia uongozi wake utachangia katika utoaji wa viwango vya ubora wa hali ya juu vya elimu kwa wanafunzi wote.

Wawaniaji watano walikuwa wameorodheshwa kwenye wadhifa huo, kutoka kwa orodha ya watu 124 waliokuwa wametuma maombi baada ya wadhifa huo kutangazwa upya kuwa wazi.

Evaleen Mitei amekuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC tangu mwezi Juni 2025, wakati Nancy Macharia alipostaafu baada ya kuhudumu kwa muda wa miaka 10.

Share This Article