Kenya yalenga fursa zaidi kwa raia wake nchini Saudia

Kenya na Saudi Arabia zimetia saini Barua ya Makubaliano ya Nia, ili kuweka mfumo wa kuimarisha ushirikiano katika kuajiri wafanyakazi Wakenya.

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya inalenga kuongeza hata zaidi, fursa za ajira kwa raia wake nchini Saudi Arabia.

Mpango huo unalenga kuwezesha raia wa Kenya kupata angalau nafasi 10,000 za ajira kila mwezi nchini humo, kupitia makubaliano mapya ya ushirikiano wa kikazi yanayolenga kupunguza gharama za kuajiriwa na kupanua fursa za ajira nje ya nchi.

Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii, Alfred Mutua, ametangaza kuwa Kenya na Saudi Arabia zimetia saini Barua ya Makubaliano ya Nia, ili kuweka mfumo wa kuimarisha ushirikiano katika kuajiri wafanyakazi Wakenya.

Makubaliano hayo, yaliyotiwa saini mjini Riyadh wakati wa mkutano wake na Naibu Waziri wa Rasilimali Watu na Maendeleo ya Jamii wa Saudi Arabia, Dkt. Abdullah bin Nasser Abuthnain, yanajumuisha mpango wa majaribio wa miezi mitatu wenye kikomo maalumu cha gharama za kuajiriwa.

Lengo la nafasi 10,000 za ajira kwa mwezi linahusisha sekta mbalimbali, zikiwemo afya, elimu, ujenzi, ukarimu, usafiri, biashara ya rejareja pamoja na mafuta na gesi.

Mutua alisema Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira, NEA, itashirikiana na mashirika ya kuajiri wafanyakazi yanayotaka kushiriki mpango huo.

Hata hivyo, alitoa onyo kali kwa Wakenya wanaotafuta ajira nchini Saudi Arabia dhidi ya kutumia mawakala wasio na leseni.

Serikali hizo mbili zitapitia matokeo ya mpango huo baada ya miezi mitatu ili kuamua iwapo utaendelezwa au kurefushwa.

Share This Article