Harambee Stars kupimana ubabe na Bafana Bafana leo

Michuano miwili ya awali kati ya Kenya na Afrika Kusini ilikuwa ya kirafiki, Afrika Kusini wakiishinda Kenya 2-0 mwaka 2011 na kuilemea tena Kenya magoli 2-1 mwaka 2012.

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya taifa ya soka ya Kenya – Harambee Stars, itashuka uwanjani Orlando mjini Johannesburg leo kuanzia saa moja usiku kwa mchuano wa tatu wa kundi D kufuzu kwa fainali za mwaka ujao za mataifa ya Afrika (AFCON).

Harambee Stars, inayoshika nanga kundini kwa alama moja kutokana na mechi mbili, italenga kupata matokeo afadhali ikijiandaa kuwakaribisha Bafana Bafana kwa mchuano wa mzunguko wa nne  tarehe 17 mwezi huu uwanjani Nyayo.

Itakuwa mara ya kwanza kwa Kenya inayoongozwa na mchezaji wa zamani  wa Bafana Bafana, Benni McCarthy,  kukutana  na Afrika Kusini katika mechi ya kimataifa ya kufuzu.

Kenya ni ya 114 huku Afrika Kusini ikishikilia nafasi ya 48 katika msimamo wa dunia (FIFA).

Michuano miwili ya awali kati ya Kenya na Afrika Kusini ilikuwa ya kirafiki, Afrika Kusini wakiishinda Kenya 2-0 mwaka 2011 na kuilemea tena Kenya magoli 2-1 mwaka 2012.

Bafana Bafana wanaoongoza kundi D kwa pointi 6 baada ya kuwashinda Guinea na Eritrea, watalenga ushindi wa tatu utakaowaweka katika nafasi bora kufuzu kwa AFCON ya mwaka ujao itakayoandaliwa na Kenya, Tanzania na Uganda.

Guinea walisajili ushindi 2-1 mjini Conakry jana usiku katika mechi nyingine ya kundi hilo na kuifikia Afrika Kusini kwa alama sita.

 

 

Share This Article