Baadhi ya viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza, wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, wameongeza kampeni za kutafuta uungwaji mkono wa Rais William Ruto ili achaguliwe tena.
Viongozi hao wamekita kampeni hiyo katika kile walichokitaja kuwa rekodi ya maendeleo ya serikali yake.
Wakizungumza katika eneo la Ndengelwa, Kaunti Ndogo ya Kanduyi, Kaunti ya Bungoma, wakati wa harambee ya kuchangisha fedha za Kanisa Katoliki, viongozi hao walisema Rais Ruto ametekeleza ahadi muhimu alizotoa katika manifesto yake ya uchaguzi.
Waliwataka wapiga kura wamuunge mkono Rais Ruto ili apate muhula wa pili, wakisema serikali yake inahitaji muda zaidi kuimarisha ajenda yake ya maendeleo na kutekeleza miradi mingine katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, viongozi hao walikosoa vikali upinzani, wakiutuhumu kwa kile walichokitaja kuwa kuendeshwa na maslahi ya kikabila, kukosa ajenda iliyo wazi na kutokuwa na uzoefu wa kutosha kuongoza nchi.
Walitoa wito kwa Wakenya kuzingatia rekodi ya maendeleo ya serikali wanapofanya maamuzi yao ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.