Mwanamuziki wa Kenya Kevin Bahati ameosolewa vikali na baadhi ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii, baada ya harusi yake kugeuka kuwa mkutano wa kisiasa.
Msanii huyo alikuwa ametangaza harusi hiyo kwa madaha akisema kiingilio ni Shilingi milioni moja kwa kila mgeni lakini kumbe, ilikuwa mkakati wa kuzindua kampeni yake ya kuwania ubunge wa Mathare mwaka 2027.
Kwa wiki kadhaa, Bahati na mkewe Diana Marua walitangaza kwa hamasa tukio lililopewa jina la The Bahatis’ Big Day, lililopangwa kufanyika Ijumaa, Novemba 6, 2026, kuadhimisha miaka 10 ya ndoa yao.
Wawili hao walipanga kuwa na wageni 100 pekee, huku kila mmoja akitakiwa kulipa Shilingi milioni moja kwa ajili ya kushiriki sherehe hiyo ya kifahari.
Hata hivyo, wageni waliofika katika ukumbi jijini Nairobi walikumbana na jukwaa la kisiasa lililokuwa na ujumbe wa “MP Mathare 2027” badala ya sherehe ya harusi waliyotarajia.
Badala ya kubadilishana viapo vya ndoa, Bahati alizindua rasmi kampeni yake ya kisiasa.
Tukio hilo limewaudhi wageni na mashabiki, huku baadhi ya watu mashuhuri, akiwemo mfanyabiashara Kenyan Prince, wakimkosoa vikali kwa madai ya kuwadanganya watu ili kufadhili kampeni yake.
Bahati alikiri kuwa kutumia simulizi la harusi kulikuwa mkakati wa kuvutia umakini wa umma na kukusanya fedha za kampeni.
Hatua hiyo imeibua maswali kuhusu uaminifu wake na huenda ikaathiri taswira yake kwa wapiga kura.