Mhubiri tata Paul Mackenzie afungwa miaka 200 gerezani

Lady Justice Kavedza alisema upande wa mashitaka ulifanikiwa kuthibitisha mauaji yote 191.

Tom Mathinji
1 Min Read

Mhubiri tata Paul Mackenzie amehukumiwa kifungo cha miaka 200 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya watu 191.

Mwanzilishi huyo wa kanisa la Good News International, alihukumiwa kifungo hicho pamoja na wenzake 28 katika Mahakama Kuu ya Mombasa.

Akitoa hukumu hiyo Lady Justice Diana Kavedza, pia aliwahukumu washtakiwa 15 miaka 160 gerezani, washtakiwa 10 walifungwa miaka 140, mshatikwa mmoja alifungwa 100 gerezani huku washtakiwa wawili wakifungwa miaka 10 gerezani kila mmoja.

Lady Justice Kavedza alisema upande wa mashitaka ulifanikiwa kuthibitisha mauaji yote 191 ambapo vifo 72 vilitokana na ukosefu wa chakula, huku vingine vikisababishwa na majeraha kwenye shingo na kichwa.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilisema kuwa vyanzo vya vifo 110 havikuweza kubainishwa kutokana na jinsi miili hiyo ilivyokuwa imeharibika.

Mnamo Oktoba 19, Lady Justice Diana Kavedza, alisema upande wa mashitaka ulithibitisha kesi dhidi ya washtakiwa wote 29.

Upande wa mashitaka kwenye kesi hiyo uliongozwa na Peter Kiprop, Jami Yamina, Victor Owiti, Ngina Mutua, Betty Rubia na Yassir Mohammed.

 

Share This Article