Vyuo vikuu nchini vimetakiwa kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kutatua changamoto kubwa zaidi zinazoikabili jamii wakati wakiwa tayari kukabiliana na mazingira ya kazi yanayobadilika mara kwa mara.
Wito huo umetolewa na Rais William Ruto leo Alhamisi wakati akikikabidhi hati Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Uongozi, ILU wakati wa hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi.
Ruto amesema vyuo vikuu na taasisi za mafunzo ya kiufundi lazima zihakikishe kuwa programu zao za kitaaluma zinaendana na hali halisi katika jamii pamoja na mahitaji yanayobadilika ya sekta mbalimbali.
Aliongeza kuwa kipimo cha mwisho cha elimu hakipaswi kuwa vyeti wanavyopata wahitimu, bali uwezo wao wa kutumia maarifa, kubuni fursa na kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya kitaifa.
“Hii ndiyo tofauti kati ya elimu inayozalisha sifa za kitaaluma na elimu inayojenga uwezo. Maarifa na utaalam ni muhimu, lakini thamani yake inajikita katika matumizi yake,” alisema Ruto.
“Shahada ya Chuo Kikuu inapaswa kuthibitisha zaidi ya kile ambacho mhitimu anakifahamu. Inapaswa kuonyesha kile ambacho mhitimu huyo anaweza kutimiza.”
Kiongozi wa taifa akitumia fursa hiyo kusema kuwa Kenya inahitaji wanasayansi wanaobuni suluhu za magonjwa, wakulima wanaobadilisha mazao ya kilimo kuwa biashara zinazonawiri, wahandisi wanaojenga kwa manufaa ya vizazi vijavyo na wajasiriamali wanaobuni nafasi za ajira.
Aliongeza kuwa mazingira yanayobadilika ya kazi, yanayochochewa na akili unde, AI, mitambo inayofanya kazi yenyewe na teknolojia za kidijitali, yanafanya liwe jambo la dharura kwa taasisi za elimu kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi.
Akirejelea ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani kuhusu “Mustakabali wa Ajira 2025″, Rais Ruto alisema kuwa inatazamiwa kwamba asilimia 39 ya ujuzi wa wafanyakazi utabadilika au kupitwa na wakati kufikia mwaka 2030.
Ni kwa misingi hiyo ndiposa alisema Kenya lazima iutaliki mfumo wa elimu unaosisitiza kukariri bila kuelewa na mitihani huku ukipuuza umakinifu, ubunifu, umaizi wa kivitendo na uvumbuzi.