Watayarishaji filamu kukongamana Kigali

Watakutana kwa awamu ya 12 ya tamasha ya filamu ya Mashariki, Novemba 23 hadi 29, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Jiji kuu la Rwanda Kigali, linatarajiwa kuwa kitovu cha tasnia ya filamu barani Afrika, Novemba 23 hadi 29, 2026.

Watengenezaji filamu, wazalishaji na wasambazaji wa maudhui kutoka mataifa mbalimbali watakutana kwa awamu ya 12 ya tamasha ya filamu ya Mashariki, almaarufu ‘Mashariki African Film Festival’.

Maudhui ya mwaka huu ya tamasha hiyo ni, “Taswira za Ustahimilivu” yaani “Reels of Resilience”.

Tamasha hiyo ya wiki moja itaonyesha filamu 80 kutoka zaidi ya nchi 30, zitakazoshindana katika vipengele vitano: Filamu Ndefu, Filamu Fupi, Filamu za Makala, Vipindi vya Televisheni na Filamu za Rwanda.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa tamasha hiyo, Tresor Senga, amesema toleo la mwaka huu litalenga kuwaunganisha watengenezaji filamu wa Afrika na wanunuzi pamoja na wasambazaji wa maudhui wa kimataifa kupitia MashaRket, soko la maudhui ya sauti na picha litakalofanyika Novemba 27 hadi 29.

Baadhi ya kampuni kubwa zinazotarajiwa kushiriki ni Canal+, MultiChoice na TV5 Monde, hatua inayotarajiwa kuwapa wazalishaji wa ndani ya Rwanda fursa za kupata masoko ya kimataifa na ushirikiano wa kibiashara.

Tamasha hiyo pia itaimarisha tuzo za Iziwacu zinazotambua mchango na mafanikio ya watengenezaji filamu nchini Rwanda.

Shughuli nyingine zitajumuisha maonyesho ya filamu, mikutano ya wadau na utoaji wa tuzo kwa ubora katika uongozaji, uigizaji, upigaji picha na usimulizi wa hadithi.

Tamasha itafungwa Novemba 29 kwa tuzo na mahafali ya wanafunzi wa Mashariki Arts Academy, taasisi inayotoa mafunzo ya vitendo kwa wanaotaka kujikita katika tasnia ya filamu.

Share This Article