Masoko ya fedha duniani yapaa baada ya ushindi wa Democrats Marekani

KBC Digital News
2 Min Read

Masoko ya fedha duniani yameshuhudia ongezeko kubwa la thamani kufuatia ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, huku bei ya mafuta ghafi ikishuka chini ya dola 100 kwa pipa.

Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent katika soko la dunia ilishuka kwa zaidi ya asilimia nane Jumatano alasiri, na kufikia takriban dola 95 kwa pipa. Hiyo ni bei ya chini zaidi kurekodiwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Kushuka kwa bei ya mafuta kunahusishwa kwa kiasi kikubwa na kauli ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, aliyesema kuwa vita dhidi ya Iran ni miongoni mwa sababu zilizochangia kushindwa kwa chama cha Republican katika uchaguzi huo.

Kauli hiyo imeonekana kuwafanya wawekezaji kutathmini upya hofu ya kuongezeka zaidi kwa mvutano katika Mashariki ya Kati.

Wawekezaji pia wamezingatia wito wa Vance wa kusitishwa kwa vita, kuchukuliwa kwa hatua za kupunguza makali ya mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha, pamoja na kupitia upya uhusiano wa Marekani na Israel.

Hali hiyo imeimarisha matumaini katika masoko ya fedha, huku baadhi ya wawekezaji wakiamini kuwa mwelekeo mpya wa kisiasa baada ya uchaguzi unaweza kupunguza uwezekano wa kuzuka kwa mzozo mkubwa wa kijeshi kati ya Marekani na Iran.

Wakati huohuo, soko la hisa nchini Marekani lilishuhudia ongezeko kubwa la thamani ya hisa.

Fahirisi ya Dow Jones Industrial Average ilifunga biashara ikiwa imepanda kwa asilimia tatu, huku S&P 500 ikiongezeka kwa asilimia 1.6 na Nasdaq, inayojumuisha kwa wingi hisa za kampuni za teknolojia, ikipanda kwa asilimia 1.4.

Taarifa ya BBC

Share This Article