Mbunge wa chama cha Democratic, nchini Marekani, Ilhan Omar, ameshinda tena uchaguzi wa kati kati ya muhula kurejea katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, akihifadhi kiti chake katika jimbo la tano la Minnesota.
Ushindi wa Omar unajiri wakati ambapo amekuwa akikabiliwa na mjadala wa kisiasa kufuatia matamshi ya Rais Donald Trump, ambaye amewahi kumtaka ajiuzulu.
Mwanasiasa huyo mwenye asili ya Somalia amekuwa mmoja wa viongozi mashuhuri katika siasa za Marekani tangu mwaka 2019, alipoweka historia kwa kuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza Waislamu kuchaguliwa katika Bunge la Marekani na mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Somalia kuhudumu katika Baraza la Wawakilishi.
Katika kipindi chake bungeni, Omar amejulikana kwa misimamo yake mikali kuhusu masuala ya sera za kigeni za Marekani, hususan ukosoaji wake dhidi ya sera za Israel na operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Mnamo Oktoba 2026, taarifa ziliripoti kuhusu uchunguzi wa Serikali ya Marekani uliogusia rekodi za uhamiaji za familia yake, suala ambalo limeongeza mjadala kuhusu mwanasiasa huyo.
Aidha, amekuwa akikabiliwa na maswali kuhusu taarifa za kifedha za familia yake na shughuli za kibiashara za mumewe.
Hata hivyo, ushindi wake wa hivi karibuni unamwezesha kuendelea kuhudumu katika Bunge la Marekani kwa muhula mwingine.
Bi. Omar hurejelea Kenya kuwa nyumbani kwani baada yake na familia yake kutoroka vita nchini Somalia, walihamia Kenya ambako waliishi kwenye kambi za wakimbizi kabla ya kuhamia Marekani.