Rais William Ruto amemwomboleza aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Jaji Mstaafu Paul Kihara Kariuki, aliyefariki leo Jumanne asubuhi.
Ruto amemtaja Kihara ambaye pia alihudumu katika wadhifa wa Rais wa Mahakama ya Rufaa, kuwa aliyefanikisha mabadiliko katika taasisi ya sheria na Idara ya Mahakama hapa nchini.
“Kwa niaba yangu na kwa niaba ya wananchi wa Kenya, natuma rambirambi kwa familia, marafiki na wafanyakazi wenzake,” alisema Rais kwenye rambirambi zake.
Kwenye ujumbe wake, Rais Ruto alitambua mchango mkubwa wa Justice Kariuki katika kuimarisha mfumo wa haki nchini, akidokeza kuwa taaluma yake ilisababisha ukuaji katika mfumo wa sheria na Idara ya Mahakama.
Ruto alitaja jukumu la Kariuki kama mwazilishi mkurugenzi wa Tasisi ya Mafunzo ya Mahakama, ambapo aliwezesha ustawi wa kitaaluma wa maafisa wa Idara ya Mahakama.
“Tutamkumbuka Jaji Kihara kama mtumishi wa umma aliyejitolea na aliyechangia kwa ukuaji na uimarishaji wa mfumo wa sheria wa Kenya na idara ya mahakama,” alisema Rais Ruto.
Jaji Kariuki aliteuliwa katika Mahakama Kuu mwaka 2003, kabla ya kujiunga na Mahakama ya Rufaa mwaka 2013. Alichaguliwa Rais wa Mahakama ya Rufaa mwaka 2013, wadhifa alioushikilia hadi mwaka 2018 alipoteuliwa Mwanasheria Mkuu.
Jaji Kihara alikuwa Mwanasheria Mkuu kati ya mwaka 2018 na 2022.