Nandy atangaza ujio wa albamu yake mpya

Inaitwa ‘911’ na itatoka Novemba 27, 2026 ikiwa na zaidi ya nyimbo 10.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Faustina Mfinanga maarufu kama Nandy, ametangaza rasmi ujio wa albamu yake mpya.

Nyota huyo alitangaza hayo katika hafla aliyoandaa usiku wa kuamkia leo akisema inaitwa ‘911’ na itatoka Novemba 27, 2026, ikiwa na zaidi ya nyimbo 10.

Akizungumza katika hafla hiyo ya kutangaza tarehe ya kutoka kwa albamu hiyo, Nandy alisema ametumia miaka miwili kuiandaa, huku akiwashirikisha Wasanii mbalimbali kutoka Tanzania, Nigeria, Uganda na Jamaica.

Mama huyo wa mtoto mmoja na mke wa msanii wa muziki Billnass alionjesha waliohudhuria hafla yake wimbo uitwao “OYA” ambao ni miongoni mwa nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo.

Nandy ambaye sasa ana umri wa miaka 33, alianza kuimba kanisani akiwa na umri wa miaka mitano pekee, lakini amefanya kazi kama mwanamuziki kwa miaka 10 sasa.

Shindano la uimbaji la Tecno Own the Stage la mwaka 2016, ndilo lilikuwa jukwaa la kwanza kubwa kwa Nandy ambapo aliibuka wa pili kwenye fainali jijini Lagos nchini Nigeria.

Mwaka 2017, alitoa wimbo wake wa kwanza uitwao ‘One Day’ ambao uliongoza safari yake katika tasnia ya muziki kabla ya kuimba kwenye Coke Studio Africa.

Albamu ambazo alitoa awali ni pamoja na The African Princess ya mwaka 2018, Wanibariki ya mwaka 2021, Taste Of Love ya mwaka 2021 na
Maturity ya mwaka 2022.

Share This Article