Kamati Kuu ya Uchaguzi nchini Israel imesisitiza kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne bado ni halali, licha ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kudai kuwa kulikuwa na wizi wa kura.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Noam Sohlberg, alisema Jumapili kuwa hata kama madai ya kuingiliwa kwa uchaguzi na mataifa ya kigeni yatathibitishwa, hayataathiri uhalali wa mchakato wa uchaguzi wala matokeo yake kwa jumla.
Sohlberg alitoa kauli hiyo akiwa pamoja na mkuu wa Shirika la Usalama wa Ndani la Israel, Shin Bet, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Chama cha Likud cha Netanyahu kilipinga matokeo hayo, kikidai bila kutoa ushahidi kuwa vyama vinavyoongozwa na Waarabu viliiba kura na kupokea ufadhili kutoka Qatar.
Hata hivyo, Qatar imekanusha madai hayo, ikiyataja kuwa kampeni ya taarifa potovu.
Kiongozi wa upinzani, Gadi Eisenkot alimshutumu Netanyahu kwa kuendesha kampeni iliyopangwa ya kudhoofisha uhalali wa matokeo.
Uchaguzi huo uliacha bunge la Israel lenye viti 120 katika mkwamo, huku muungano wa Netanyahu ukipata viti 53 dhidi ya 48 vya upinzani.
Vyama vinavyoongozwa na Waarabu vilipata jumla ya viti 19, idadi ya kihistoria, na kuacha pande zote mbili bila wingi wa kutosha kuunda serikali pekee.