Rubio akanusha madai ya serikali kumsaidia Bolsonaro Kukimbilia Marekani

Alisema Marekani haikuhusika kupanga safari ya Bolsonaro na kwamba alikuwa na viza ya awali na Rais Trump aliamua kumruhusu kuingia Marekani.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kwamba utawala wa Rais Donald Trump haukumsaidia mgombea wa urais wa Brazil aliyeshindwa, Flavio Bolsonaro, kuondoka nchini humo na kukimbilia Marekani.

Bolsonaro alihamia Marekani baada ya kushindwa katika duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya Rais Luiz Inacio Lula da Silva.

Bolsonaro aliwasili Miami, Florida, Jumatano, siku moja baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kutangaza kuwa yeye na familia yake watapatiwa viza za kuingia nchini humo kufuatia kushindwa katika uchaguzi wa Oktoba 25, matokeo yaliyokwenda kinyume na mfululizo wa ushindi wa wagombea wa mrengo wa kihafidhina huko Amerika ya Kusini.

Bolsonaro anakabiliwa na uchunguzi nchini Brazil kuhusu madai ya ufisadi, utakatishaji fedha na kukwepa kulipa kodi. Kabla ya kuondoka nchini humo, alikuwa ameamriwa kukabidhi pasipoti yake baada ya polisi kumtaja kuwa mtu anayeweza kutoroka.

Akizungumza na wanahabari Jumamosi mjini Atlanta, Georgia, Rubio alisema Marekani haikuhusika katika kupanga safari ya Bolsonaro akiongeza kwamba alikuwa na viza ya awali na Rais Trump alifanya uamuzi wa kumruhusu kuingia Marekani.

Rubio alisisitiza kuwa serikali ya Marekani haikuhusika moja kwa moja katika hatua zozote zilizochukuliwa kumwezesha kuondoka Brazil.

Kwa upande wake, Rais Trump, ambaye awali alikuwa ametaja uchaguzi wa Brazil kuwa ulioandaliwa kwa udanganyifu, alionyesha kumuunga mkono Bolsonaro na kusema anaweza kubaki Marekani kwa muda wowote anaotaka.

Share This Article