Washukiwa Watano wa ulanguzi wa mihadarati wakamatwa na DCI

Walikamatwa kwenye oparesheni tofauti katika kaunti za Kisumu, Kisii na Nairobi.

Marion Bosire
2 Min Read

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI imewakamata washukiwa watano na kunasa zaidi ya kilo 582 za bangi inayoshukiwa kuwa mihadarati katika operesheni kali za kupambana na biashara ya dawa za kulevya katika kaunti za Kisumu, Kisii na Nairobi.

Huko Kisumu, maafisa wa upelelezi walinasa gari aina ya Toyota Axio la rangi ya dhahabu, lenye nambari ya usajili KCM 214Q, katika mzunguko wa barabara wa Kisumu Boys.

Dereva alitoroka baada ya kukaidi agizo la polisi la kusimama, huku abiria aliyekuwa naye, Frida Night Odour, wa umri wa miaka 21, akikamatwa.

Upekuzi wa gari hilo ulifichua kilo 282.55 za bangi iliyokuwa imefungashwa katika magunia saba na kiasi kingine kilichokuwa kimewekwa ovyo ndani ya gari.

Maafisa pia walipata katoni 40 za sigara za Supermatch zinazoshukiwa kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru.

Katika kaunti ya Kisii, maafisa walivamia nyumba katika kituo cha biashara cha Keumbu baada ya kupata taarifa kutoka kwa mwananchi na kunasa takriban kilo 300 za bangi.

Elijah Amisi Mogire, wa umri wa miaka 32, alikamatwa.

Wakati huo huo, katika mtaa wa Jericho jijini Nairobi, polisi waliwakamata washukiwa watatu, Noah James Kariuli, Calvin Malibo na Brian Ndolo.

Maafisa walipata misokoto 1,002 ya bangi iliyokuwa imefichwa kwenye mfuko mweusi wa plastiki.

DCI ilisema vielelezo vyote vilivyopatikana vimehifadhiwa huku washukiwa hao watano wakisalia mikononi mwa polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article