Raia wa kigeni amepigwa na umati hadi kufariki katika Jiji la Durban nchini Afrika Kusini, huku taharuki ikiendelea kutanda dhidi ya raia wa kigeni wanaoishi nchini humo.
Kulingana na Polisi, umati wa watu ulimfumania raia huyo akiwa amesimama kando ya barabara katikati mwa jiji la Durban na kumua papo hapo.
“Mwathiriwa alishambuliwa na takriban watu 50 na alithibitishwa amefariki katika eneo la mkasa,” ilisema taarifa ya polisi.
Hata hivyo, polisi hawakuthibitisha uraia wa mwathiriwa huyo, lakini walisema umri wake ni miaka 30 au 40, huku wakiendelea kuwatafuta washukiwa wa shambulizi hilo.
Jiji la Durban limekuwa kitovu cha mashambulizi ya raia wa kigeni, huku ghasia na uporaji wa mali zikiripotiwa wakati wa maandamano dhidi ya raia wa kigeni wiki tatu zilizopita.
Maandamano ya kuitaka serikali iwafurushe wahamiaji haramu nchini humo zilianza mwezi Juni, baadhi yazo yakigeuka na kuwa ghasia.