Serikali yaapa kuangamiza ufisadi katika utumishi wa umma

Martin Mwanje
1 Min Read
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei

Serikali imeelezea dhamira yake ya kukabiliana vikali na ufisadi katika utumishi wa umma kama sehemu ya jitihada zake za kuboresha utoaji huduma kwa raia. 

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema kwamba serikali imeazimia kubadilisha mbinu katika kukabiliana na uovu huo anaosema umeathiri utekelezaji wa maendeleo nchini.

Kulingana naye, ili kukabiliana na ufisadi ipasavyo, serikali imetekeleza mfululizo wa mikakati ikiwa ni pamoja na kuimarisha taasisi za upelelezi na kuwatumia maafisa wa utawala wa serikali kuu waliopo kote nchini.

“Tutaziruhusu taasisi za upelelezi kutekeleza majukumu yao, EACC na DCI wataendelea na majukumu yao ya kufanya upelelezi na kubaini ni nini hasa kilichotokea katika hali ambapo kuna ufisadi,” amesema Koskei.

Aliyasema hayo leo Ijumaa alipoongoza mkutano wa usalama uliohudhuriwa na maafisa waandamizi wa utawala katika shule ya mafunzo ya serikali katika eneo la Lower Kabete.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo na kuangazia upitiaji upya wa utendakazi wa taasisi za serikali wakati wa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Wakati wa mkutano huo, washiriki walijadiliana mbinu za kukabiliana vilivyo na ufisadi ambao umejipenyeza hadi idara mbalimbali za serikali.

 

Website |  + posts
Share This Article