Ruto awapongeza wanamichezo walioiweka Kenya katika ulingo wa Kimataifa

Alisema uwekezaji katika miundombinu ya michezo, utahakikisha utunzi wa talanta, kubuni nafasi za kazi na kudumisha nafasi katika michezo ya kimataifa.

Tom Mathinji
2 Min Read

Wanariadha waliopeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya kimataifa, wametajwa kuwa mashujaa wa taifa hili kutokana na bidii yao ya kuhakikisha ustawi wa taifa hili.

Kwenye sherehe ya kuadhimisha Siku Kuu ya Mashujaa iliyoandaliwa kwa pamoja na kaunti za Nandi, Elgeyo Marakwet na Uasin Gishu, Rais William Ruto, aliwataja wanariadha hao kuwa mfano bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo vya taifa hili.

“Kuanzia Faith Kipyegon na Beatrice Chebet, hadi Peres Jepchirchir, Faith Cherotich na Lilian Odira, mabingwa wetu wameendelea kuipeperusha kwa fahari bendera ya Kenya na kuwapa motisha vijana wetu,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto aliongeza kuwa, “Tunatambua kila kila mwanariadha ambaye amewakilisha taifa letu, ikiwemo wale ambao majina yao hayawezi kuonekana kwenye kumbukumbu lakini kujitolea kwao kunaimarisha azma yetu ya riadha”.

Kuhusu mchezo wa soka, kiongozi wa taifa alisema wakati umewadia sasa kwa Kenya kuikaribisha ulimwengu, wakati huu ambapo itakuwa miongoni mwa mataifa yanayoandaa mashindano ya kuwania kombe la Mataifa Bingwa Afrika mwaka 2027.

“Tunapojiandaa kuandaa kombe la kuwania taifa bingwa barani Afrika kwa ushirikiano na Uganda na Tanzania, tunawekeza katika vifaa vya kisasa vya riadha ukiwemo Uwanja wa Kimataifa wa Raila Odinga pamoja na kuweka vifaa vya kisasa katika Uwanja wa Kimataifa Kasarani,” alidokeza Rais Ruto.

Alisema uwekezaji katika miundombinu ya michezo, utahakikisha utunzi wa talanta, kubuni nafasi za kazi na kudumisha nafasi katika michezo ya kimataifa.

Share This Article