Kenya yamaliza michezo ya Olimpiki ya chipukizi kwa dhahabu nne

Wanariadha saba walioshiriki michezo hiyo waliwasili nyumbani jana Jumatano usiku baada ya kufanya vyema, wakizoa medali 5; dhahabu 3 na fedha 2.

Dismas Otuke
2 Min Read

Kenya ilizoa jumla ya nishani sita  katika makala ya nne ya michezo ya Olimpiki kwa chipukizi yanayoelekea ukingoni mjini Dakar, Senegal.

Wanariadha saba walioshiriki michezo hiyo waliwasili nyumbani jana Jumatano usiku baada ya kufanya vyema, wakizoa medali 5; dhahabu 3 na fedha 2.

Kenya ilinyakua jumla ya nishani nne za dhahabu zikiwemo tatu katika fani ya riadha huku dhahabu nyingine moja ikinyakuliwa na timu ya raga kwa wanawake saba upande.

Enock Tuitoek na Faith Rono walishinda dhahabu katika mbio za mita 3,000 huku Abigae Kosgei akiongeza dhahabu nyingine katika mita 2,000 kuruka viunzi na maji.

Nishani mbili za fedha zilitwaliwa na Wesley Kipkech katika mita 2,000 kuruka viunzi na maji na Abigael Chepkirui katika mita 1,500.

Kenya inawakilishwa na jumla ya wanamichezo 51 katika mashindano hayo yanayoandaliwa Afrika kwa mara ya kwanza.

China ni ya kwanza katika msimamo wa nishani kwa medali 30; dhahabu 16, fedha 8 na shaba 6, ikifuatwa na Japani kwa dhahabu 9, fedha 8 na shaba 9.

Urusi ni ya tatu kwa nishani 14; dhahabu 8, fedha 4 na shaba 2 ikifuatwa na Misri kwa dhahabu 6, fedha 1 na shaba 5.

Ethiopia inakamilisha orodha ya mataifa matano bora kwa dhahabu 5 na fedha 3.

Share This Article