Uchumi wa Kenya ni wa saba kwa ubora Afrika, asema Rais Ruto

Rais alisema utawala wake umefanikiwa kuthibiti ubadilishanaji wa sarafu, mfumuko wa bei, kuboresha nafasi za kupatikana kwa mikopo na kurekebisha masoko ya mtaji.

Tom Mathinji
2 Min Read
William Ruto - Rais wa Kenya.

Rais William Ruto amesema uchumi wa taifa hili umeimarika katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kutokana na hatua kabambe zilizochukiliwa na serikali yake.

Kiongozi wa taifa alisema utawala wake umefanikiwa kuthibiti ubadilishanaji wa sarafu, mfumuko wa bei, kuboresha nafasi za kupatikana kwa mikopo na kurekebisha masoko ya mtaji.

Akizungumza leo Jumanne alipoongoza taifa kuadhimisha Siku Kuu ya Mashujaa iliyoandaliwa katika kaunti ya Uasin Gishu, Ruto alisema utoaji mikopo kwa sekta ya kibinafsi umeimarika, akiongeza kuwa thamani ya soko  la hisa imeongezeka maradufu kutoka shilingi trilioni 2 hadi shilingi trilioni 4.

“Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni umeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitatu, kutoka dola bilioni 1.5 mwaka 2022 hadi dola bilioni 3.2 mwaka 2025, na sasa uchumi wa taifa la Kenya ni wa saba kwa ubora barani Afrika,” alisema Rais Ruto.

Wakati huo huo, Rais alisema serikali imepanua nafasi ya kupatikana kwa mikopo kwa masharti nafuu kwa mamilioni ya wakenya ambao hapo awali  walitengwa kutoka kwa huduma rasmi za kifedha.

“Kupitia Hazina ya hasla, zaidi ya Wakenya milioni 10 sasa wanapata mikopo ya mara kwa mara huku shilingi bilioni 98 zikitolewa bila ya kuwa na dhamana yoyote,” alidokeza Rais Ruto.

Aidha, alisema ifikapo mwisho wa mwaka 2026, serikali itawekeza shilingi bilioni tano zaidi kwa hazina hiyo ya hasla, ili kupanua nafasi ya kupata mikopo na kuimarisha biashara nyingi zaidi.

Share This Article