Trump atetea kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo dhidi ya Urusi

Amemshutumu Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy pia kwa kutokuwa na nia ya kumaliza vita hivyo.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais Donald Trump wa Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump, ametetea uamuzi wa kuondoa kwa muda baadhi ya vikwazo dhidi ya Urusi, akisema anataka kuhakikisha Nchi hiyo inaendelea kushiriki mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine.

Wakati huo huo, amemshutumu Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy kwa kile alichokitaja kuwa kutokuwa na nia ya kumaliza vita hivyo.

Trump alitoa kauli hiyo jana Jumapili kupitia mtandao wake wa Truth Social, akijibu ukosoaji kuhusu uamuzi wake wa kuzuia utekelezaji wa vikwazo kadhaa dhidi ya Urusi siku chache kabla ya kuanza kutekelezwa.

Trump alisema anaendelea kujadiliana kuhusu amani kati ya Urusi na Ukraine na hataki kuchukua hatua zinazoweza kuifanya Moscow kujiondoa kwenye meza ya mazungumzo.

Uamuzi huo umesababisha mvutano mkubwa wa kidiplomasia kati ya Trump na Zelenskyy katika wiki iliyopita.

Zelenskyy, ambaye nchi yake ilivamiwa kwa kiwango kikubwa na Urusi mwaka 2022, alisema kuondolewa kwa vikwazo hivyo kutadhuru Ukraine na kuimarisha juhudi za kijeshi za Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Akizungumza kwenye mahojiano, Zelenskyy alimwelezea Putin kama mchokozi aliyeikalia nchi yake na kuua raia, wakiwemo watoto. Alisema anatumaini Trump atakuwa na msimamo wazi kuhusu suala hilo.

Trump alisisitiza madai yake kwamba Zelenskyy hataki kumaliza vita, akidai Ukraine inaendelea kushambulia viwanda vya kusafisha dizeli nchini Urusi licha ya athari zinazoweza kujitokeza katika soko la kimataifa la mafuta hayo.

Share This Article