Nigeria, Afrika Kusini, Burkina Faso zakataa wakimbizi wanaofurushwa Marekani

Nigeria imetaja changamoto nyingi za ndani huku Burkina Faso ikipinga kutumiwa kuhifadhi wanaokataliwa na nchi nyingine.

Marion Bosire
2 Min Read
Donald Trump - Rais wa Marekani

Mataifa ya Nigeria, Afrika Kusini na Burkina Faso katika bara Afrika, yamekataa ombi la Marekani la kupokea wahamiaji wa mataifa mengine wanaofukuzwa nchini humo.

Nchi hizo zimeelezea wasiwasi kuhusu usalama, mamlaka ya kitaifa na uwezo wa kuwahudumia watu hao.

Marekani imekuwa ikitafuta nchi za Afrika zitakazowapokea wahamiaji wasioweza kurejeshwa moja kwa moja katika nchi zao za asili, wakiwemo baadhi ya watu wenye rekodi za uhalifu au kesi ambazo hazijakamilika.

Nigeria imesema tayari inakabiliwa na changamoto nyingi za ndani, huku Burkina Faso ikipinga kutumiwa kama eneo la kuwapeleka watu ambao nchi nyingine hazitaki kuhifadhi. Afrika Kusini nayo imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa hatari za kiusalama.

Hata hivyo, Uganda, Rwanda, Eswatini, Sudan Kusini na nchi nyingine za Afrika zimetajwa kuwa tayari kushirikiana na Marekani katika mpango huo, ingawa masharti ya makubaliano yanatofautiana.

Mpango huo umekosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, likiwemo Human Rights Watch, ambalo limeonya kuhusu uwezekano wa wahamiaji kuzuiliwa kiholela, kunyimwa msaada wa kisheria au kurejeshwa katika nchi wanakoweza kukabiliwa na mateso.

Hatua ya nchi hizo tatu imeibua mjadala kuhusu namna serikali za Afrika zinaweza kushirikiana na Marekani bila kuhatarisha usalama wa wananchi, haki za wahamiaji na uhuru wa kufanya maamuzi ya kitaifa.

hazitaki kuhifadhi. Afrika Kusini nayo imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa hatari za kiusalama

Share This Article